KILIMO CHA NYANYA CHUNGU
Zao hili pia hujulikana kwa jina la "Nyanya Chungu", "Ngogwe" au
"Ntongo". Huu ni mmea wa kitropiki, na kustawi kwake karibu ni sawa na
bilinganya.
Mmea hukua na kufikia urefu wa
meta moja hadi moja na unusu na matawi na majani yake hufanya kichaka.
Nyanya mshumaa zinaweza kuwekwa katika makundi mawili: yaani aina itoayo
matunda madogo madogo na machungu sana na aina itoayo matunda makubwa
na machungu kidogo.
Rangi ya matunda huwa kijani
kibichi au kijani-njano, au njano-nyeupe, na yakipevuka kabisa hugeuka
mekundu. Matunda yafikia hatua ya kupevuka huwa hayafai tena kuliwa, ila
kwa kutoa mbegu za kupanda. Matunda hupikwa au kukaangwa na kufanywa
mchuzi, au huchanganywa na mboga zingine. Pia hupikwa pamoja na ndizi.
Kupanda: Miche huoteshwa kwa kupanda mbegu ambayo husiwa kwenye
kitalu na kutunzwa kama mazao mengine. Miche ifikiapo kimo cha sentimeta
10 hadi 15 hupandikizwa bustanini, kwa umbali wa sentimeta 90 kwa 90,
hadi 120 kwa 120; hii kutegemeana na ukubwa wa kichaka chake. Mimea ya
"Ngogwe" hutunzwa kama bilinganya, huhitaji ardhi yenye rutuba na unyevu
wa kutosha. Mazao huanza kuvunwa miezi miwili baada ya kupandikizwa, na
uvunaji huendelea kwa muda mrefu kidogo.
Maadui: Nyanya Mshumaa ni mmea mgumu, kwani unaweza kustahimili
upungufu wa maji kuliko aina nyingine za Mboga. Vile vile haushambuliwi
sana na baadhi ya Magonjwa yasababishwayo na mvua au uchepechepe mkubwa.
Ingawa yako magonjwa na wadudu ambao hushambulia zao hili, madhara ya
si makubwa sana kiasi cha kutisha au kumkatisha tamaa mkulima. Usafi wa
bustani na kubadilisha mpando wa mazao, vinaweza kuondoa tishio hilo.
Kuvuna: Mboga huvunwa wakati zikiwa bado mbichi. Ili ziweze kukaa
kwa muda mrefu (hata majuma mawili) bila kuharibika, inapendekezwa
kuzichuma pamoja na sehemu ya vikonyo vyake. Vikonyo hivyo hukobolewa
wakati wa kuzitayarisha kupikwa. Kwa hiyo, zao hili linaweza
kusafirishwa hadi masoko ya mbali bila kuharibika.
Mkulima ongeza uzalishaji katika mazao ya mboga mboga ukuze uchumi wako.
KILIMO CHA NYANYA CHUNGU
Reviewed by darasa uchumi
on
11:32:00 AM
Rating:
No comments